MWONGOZO WA UTOAJI MIKOPO KWA 2019/2020
Bodi ya Mikopo ya WanafunzI wa Elimu ya Juu (HESLB)
imetangaza mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2019/2020
ikiwa ni maandalizi ya kukaribisha maombi ya mikopo kwa mwaka ujao wa masomo wa
2019/2020.
Mwongozo huo wa kina unataja sifa za waombaji, utaratibu wa
kuomba mikopo, na melekezo mengine muhimu, na unapatikana kwenye tovuti hii.
Kuupakua mwongozo
HESLB inatarajia kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya
juu kwa mwaka wa masomo 2019/2020 kuanzia Juni 25, 2019 hadi Agosti 15, 2019,
ikiwa imetenga kipindi cha majuma mawili kuwapa fursa waombaji wa mikopo
watarajiwa kusoma kwa makini mwongozo huo na kujiandaa kuomba mikopo.
Aidha, HESLB inawakumbusha wanafunzi wanaotarajia kuomba
mikopo ya shahada ya kwanza kuzingatia mambo yafuatayo:
Kuwa na nakala za vyeti vifuatavyo vilivyothibitishwa na
Wakili, Hakimu
a). Cheti cha Kidato cha Nne;
b). Cheti cha Kidato cha Sita;
c). Cheti cha Stashahada (Diploma);
d). Cheti cha kuzaliwa
e). Cheti cha kifo cha mzazi au wazazi.
Nakala za vyeti (d na e) ziwe zimethibitishwa na Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii
Zanzibar.
2. Aidha, Wanafunzi wenye ulemavu au wenye wazazi wenye
ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga
Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali;
3. Wanafunzi ambao walifadhiliwa masomo yao katika ngazi ya
Sekondari au Stashahada (Diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo
kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao;
4. Waombaji wote wa mikopo wanakumbushwa kuusoma kwa makini
mwongozo wa 2019/2020 na kuuzingatia.
Kwa maelezo zaidi, tuandikie kwa
Baruapepe: adcp@heslb.go.tz